Tuesday, March 28, 2017

Tuko katika maonesho njoo Tuunge mkono




WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kutumia vifungashio vyenye ujazo sahihi ili kufikia soko la kimataifa.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam leo na Kaimu Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Irene John wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) cha Wajasiriamali Wanawake Tanzania (TASWE).
John alisema wajasiriamali wengi nchini wamekuwa wakishindwa kuyafikia masoko ya kimataifa kutokana na vifungashio vyao kukosa vipimo sahihi.
Huwezi kufikia soko la kimataifa kama utatumia vipimo sahihi kama kitu ni cha kilo moja weka kwenye ujazo wa kilo moja kwa kufanya hivi utaweza kujitangaza na kuifanya biashara yako kuwa kwenye kiwango sahihi, alisema John na kuongeza kuwa matumizi ya ujazo usio sahihi sio tu yanawanyima kujulikana katika soko la kimataifa, bali yanaweza kuwaumiza wajasiriamali au walaji.
Kuna ambao wanatumia chupa za maji kufungasha bidhaa zao, lakini hawajui kama maji ni mepesi na ujazo wake wake hauwezi kulingana na asali hivyo unaweza kujinyima wewe kama mjasiriamali au ukamnyima mlaji, aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWE, Anna Matinde alisema maonesho hayo yameshirikisha wajasiriamali 192 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Comoro, Uganda, Rwanda, Kenya na wenyeji Tanzania.
Matinde alisema maonesho hayo ni muhimu kwa kuwa yanasaidia nchi zilizoshiriki kubadilishana uzoefu katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.
Aidha, alisema ili kuhakikisha elimu ya ujasirimali inafika katika nchi za Afrika Taswe inajenga chuo cha mafunzo Comoro ili kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa bidhaa za Tanzania.
Naye Ofisa Ukuzaji wa Biashara kutoka Mamlaka ya Uendelezaji Biashara Tanzania (Tantrade), Judith Matage alitoa mwito kwa wajasiriamali hao kuyatumia maonesho hayo kujitangaza na sio kuuza bidhaa pekee.
Hii ni fursa lazima muitumie sio muuze tu sambazeni mawasiliano kwa wajasiriamali kutoka nchi nyingine kwa kufanya hivi kutawaongezea kujitangaza katika nchi mbalimbali, alisema Matage.