Saturday, February 13, 2016

Mwanaume kuwa na ngozi nzuri huleta furaha, kujiamini

HAIJALISHI unafanya kazi kwenye mazingira gani lakini cha muhimu ni kuzingatia unatunza vizuri ngozi yako ya uso ili kuboresha muonekano wake. Mwanaume kuwa na ngozi nzuri huleta, furaha na kujiamini pia . Muonekano mzuri usoni ni miongoni mwa mambo ambayo wanaume wanatakiwa kuyazingatia na hili linawezekana kama utaijali ngozi yako na utanashati kwa jumla. Kuna wanaume ambao hawana hata muda wa kujiangalia kwenye kioo labda kwa kudhani kuwa mambo hayo yanatakiwa kufanywa na wanawake jambo ambalo si sawa sawa. Kuna mambo mengi ambayo mwanaume anatakiwa kufanya ili aweze kuonekana na muonekano mzuri. Miongoni mwa mambo hayo ni kuhakikisha unasafisha uso na kutakata, hapa unaweza kutumia taulo laini kwa kupaka kidogo sabuni na kisha safisha uso taratibu na baadaye unasuuza uso na kuufuta. Pia unaweza kutumia cleanser ambayo ni maaluma kwa ajili ya kusafisha uso. Si jambo la ajabu unapopita kwenye saluni na kukuta wanaume wakisafishwa uso au kufanya scrubing ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikisaidia kuondoa madoa usoni, mafuta na kufanya ngozi ipendeze. Unaposafisha uso unaruhusu vitundu vya kutolea hewa kubaki wazi na hivyo kufanya ngozi kuwa na afya nzuri na hata muonekano wake kuwa bora zaidi. Jitahidi kusaifisha uso na kufanyia scub uso wako japo angalau mara mbili kwa wiki jambo hili kwa kiasi kikubwa husaidia kuondoa seli zilizokufa kwenye ngozi. Pia hufanya kuwa laini na ya kuvutia. Unaweza kupaka loshen au cream za kiume ambazo zipo madukani kwa ajili ya kuboresha zaidi ngozi yako.