Saturday, August 23, 2014

Tumia limao kuondoa madoa meusi usoni




KUMEKUWA na sababu mbalimbali zinazofanya watu kutokuwa na ngozi zisizokubalika.Mbali na hali ya hewa pia matumizi ya pombe na sigara hata matumizi ya cream kali ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu bila kujua madhara yake kumechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.
Ngozi kwa kawaida inatakiwa ijitengeneze yenyewe na si kuitengeneza kwa vipodozi kama wengi wanavyodhani. Ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi kunywa glasi nane za maji kwa siku ni njia nzuri kama unataka kuwa na ngozi nzuri isiyo na madoa wala ukavu ambao haupendezi.
Wengi wanaacha kula mbogamboga na matunda kwa wingi hata kutokunywa maji ya kutosha na badala yake wamekuwa akitegemea kuwa na ngozi nzuri jambo ambalo ni gumu.Mara kadhaa tumeshuhudia watu wanaopaka cream kali wakiwa kama wameungua usoni huku uso na mwili ukionekana kuwa makavu jambo ambalo linaashiria kuwa kupaka cream  si suruhisho la kuwa na ngozi nzuri.
Kuna watu wamekuwa na ngozi za asili na hata unapowauliza baadhi yao hawajawahi kupaka cream hata siku moja na bado wana ngozi nzuri zinazovutia hao wamekuwa wakila kwa ajili ya kuhakikisha wanatengeneza ngozi zao kutoka ndani.
Pia wengi wanaharibu ngozi zao na kuwa na madoa kutokana na kutumia make up kwa muda mrefu  na hata anapogundua kuwa ana tatizo la madoa amekuwa akijaribu kutumia cream nyingine kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo jambo ambali linazidisha madhara kwenye ngozi.
Unaweza kutibu ngozi yenye madoa usoni  pia mashavuni kwa kujitibu na juisi ya limao.
Namna ya kufanya
Chukua  limao lioshe na kisha likamue na kuchuja mbegu zake. Weka juisi hiyo kwenye kikombe na kisha tafuta kitambaa laini  kichovye kwenye juisi ya limao na dondoshea juisi ya limao kwenye sehemu zenye tatizo.
Kaa  kama dakika tano kisha usha uso kwa maji safi.Pia unaweza kuchanganya na asali mbichi  na maji ya limao husaidia pia kuondoa madoa usoni.
Limao lina sifa kubwa ya kuzuia harufu pia unaweza kulitumia katika kuondoa harufu kali ya jasho mwilini  na husaidia kuondoa weusi kwenye kwapa, chini ya macho, mapajani pia.
Chukua kipande cha limao  weka sukari kidogo, sugua.Unatakiwa kutumia kwenye kwapa ambalo ni safi, vizuri kutumia njia hii kabla na baada ya kuoga.

Wednesday, August 20, 2014

Unatunzaje mikono yako?

Ili kuweka mikono yako kuwa na muonekano mzuri wa asili na kuwa laini unatakiwa kuipa uangalizi wa kutosha ukiwa nyumbani. Mikono imekuwa ikitumika na kazi nyingi za nyumbani hata ofisini na wakati mwingine tumekuwa tukishika vitu ambavyo vinasababisha mikono kuwa migumu na hata iliyobabuka.
Watu wengi wamekuwa wakitengeneza nyuso zao na kusahau kabisa habari za kutunza mikono kitu ambacho si sawa sawa.
Unatakiwa kujifunza vitu gani vinatakiwa ili kuweza kuiweka mikono yako katika hali nzuri ikiwemo aina ya scrub na moisturizer ambayo itafanya mikono yako kuwa katika hali nzuri kila wakati.
Unaweza kutengeneza mikono yako ukiwa nyumbani  au hata saluni lakini kama utafanya mara moja kwa wiki utakuwa na mikono ambayo iinaonekana vizuri.
Ili kutengeneza mikono yako unatakiwa kuwa na nail file (tupa ya kucha), brashi ya mikono, kitu cha kukatia kucha (hata webe unafaa) losheni ya mikono, taulo sabuni na maji wa vuguvugu.
Unatakiwa kuosha mikono na ukate kucha na kisha anza kuzisugua taratibu kwa kutimua tupa.
Kisha weka maji ya vuguvugu kwenye beseni na tumbukiza mikono kaa kwa muda wa dakika tano ili kuwezesha ngozi ya mikono kulainika.
Kisha anza kusugua mikono taratibu unaweza kutumia kitambaa laini ila unachotakiwa kuhakikisha unasafisha hadi sehemu za katikati ya vidole baada ya hapo suuza mikono yako na ufute kwa taulo halafu paka lotion ya mikono. Njia nzuri pia ya kutunza mikono ni kuhakikisha unakula chakula chenye kulainisha mwili na kunywa maji mengi.
Kama unakuwa hujali mwili wako na hunywi maji mengi unaweza kuwa na mikono mikavu.