Tuesday, August 3, 2010

Sifa ya mwanamke ni kujipamba


MWANAMKE ni ua. Ni msemo wa muda mrefu ambao tulizaliwa na tukaukuta.
Msemo huu ulikuwa ukimaanisha kuwa, mwanamke atapendeza iwapo atajipamba na kuonekana bomba kila wakati ndiyo maana akafananishwa na maua, hakuna asiyejua thamani ya maua hasa pindi yanapochanua na kuonekana mazuri huku mengine yakitoa harufu nzuri.
Dunia ya leo ni ulimwengu wa wanawake wanaojipamba na kuonekana warembo zaidi.
Wanawake ambao wana uzuri wa asili hasa wale ambao wametunza ngozi zao nyeusi za asili hupendeza sana kama watajipamba kwa vitu vya asili kama kuvaa hereni, mikufu au bangili zilizotengenezwa kwa vitu vya asili kama vifuu vya nazi, magome ya miti au kutengenezwa kwa kutumia shanga.
Wakati huu wanawake wenye uwezo kifedha wamekuwa wakitumia fedha zao kujipamba kwa mapambo ya gharama kubwa kama kuvaa mikufu na saa zenye za dhahabu na hata madini mengine yenye thamani kubwa kama almasi.
Uvaaji wa mikufu, hereni, bangili ni mambo ambayo mwanamke anatakiwa kuyazingatia ili kuweza kuongeza urembo wake.
Wengi wetu tumekuwa tukisahau kutumia vitu hivi katika mavazi yetu.
Vitu hivi vimekuwa vikisaidia sana kuboresha maisha yetu ya urembo kutokana na kuwa unapovaa hereni, mkufu au bangili iliyofanana na nguo uliyovaa hii itasaidia uonekana nadhifu zaidi kuliko unavyofikiri.
Mwanamke ambaye amekuwa akipangilia mavazi yake amekuwa akionekana nadhifu kuliko yule ambaye amekuwa akiweka mwilini kila aina ya rangi na kufanya muonekano wake usiwe mzuri.
Kuna mapoambo mengi siku hizi tena kwa gharama nafuu sana cha kuzingatia ni kucheza na rangi, ukijua namna ya kupangilia rangi za mavazi yako na mapambo yako utakuwa umefanikiwa sana katika kufanikisha muonekano wako uwe mzuri.
Kitu kingine cha kuzingatia ni kuwa, unapoamua kupangilia rangi za mavazi yako hakikisha kuwa mvazi hayo hayawi kwenye rangi za kung’aa sana hasa pindi mavazi hayo ni ya kuvaliwa wakati wa mchana.

No comments:

Post a Comment