Thursday, December 16, 2010

Umaridadi wa wanaume uko mikononi mwa wanawake


LEO nataka tukumbushane kitu kimoja nacho ni jinsi ya kumfanya mwenzi
wako aonekane maridadi wakati wote. Hapa nazungumzia wale walio katika
mahusiano ya kudumu ambao wanaishi pamoja.
“Nikiamka asubuhi jambo la kwanza ni kumuandalia mume wangu maji ya
kuoga, nahakikisha nguo zake zimepigwa pasi, viatu vimeng’arishwa,
soksi ziko safi, na akivaa lazima nimfunge tai, na nguo za kazini mimi
ndiye nachagua siku hiyo avae nguo gani” anasema Mama mmoja mkazi wa
Kimara Jijini Dar es Salaam.
Sikiliza na hii “ Mimi mume wangu huwa anaandaa nguo zake mwenyewe
anafua, apige pasi au asipige shauri yake, aoge asioge atajijua, huo
muda sina kabisa siku hizi” anasema mwanamke mmoja Mkazi wa Buguruni
Jijini Dar es Salaam.
Siku zote tumekuwa tukisisitiza urembo kwa wanawake na utanashati kwa wanaume.
Mmoja ya jukumu la mwanamke ni kuhakikisha kuwa, mwanaume wake anakuwa
maridadi na mwenye kuvutia. Jaribu kuangalia ni nguo za aina gani mume
akivaa zinampendeza na hapo unaweza kumchagulia shati na suruali
ambazo rangi zake zinaendana na hata akivaa zitamfanya apendeze.
Pia suala zima la kufua na kupiga pasi vizuri ni moja ya njia ya
kuonyesha kuwa unamjali na unamjengea namna ya kujiamini
zaidi.Utunzaji wa soksi ikiwemo ufuaji wa nguo za ndani ni jambo
linalosisitizwa sana kwani wanaume wengi wanaonekana kutojali sana
vitu hivyo ama kutokana na muda au kwa kukosa ushirikiano wa wenzi wao
katika kutunza na kufanyia usafi aina hizo za nguo.
Jamani mwanaume akiwa maridadi au mtanashati huwa anamvutia kila mtu
na zaidi sifa zinakwenda kwa mkewe ambaye anaaminika kuwa ni chanzo
cha mwanaume kuwa msafi.
Jenga mazingira ya kujali usafi wa nguo za mwenzi wako ili kuhakikisha
kuwa kila kitu kinakwenda sawa.
Pia kuna wanawake wengi ambao ni wajuzi wa kufunga tai, kama hilo bado
hulifahamu tafuta mtu ambaye atakufundisha namna bora ya kufunga tai
ili uweze kumpendezesha mume wako.
Kama unapita dukani au sehemu zinakouzwa nguo si vibaya kama unaona
kuna nguo inaweza kumfaa mwenzi wako mna ukahakikisha kuwa akivaa
anapendeza usisite kununua kwani itakuwa ni zawadi nzuri sana kwake.
Jaribu kuwa na tabia ya kumvika mwenzi wako, si kuacha kila kitu
afanye yeye kuanzia kufua, kupiga pasi na hata kung’arisha viatu.
Ni vizuri kama utaamua kuhakikisha kuwa, unamuaandaa mume wako kabla
ya kwenda kazini kisha na wewe kuendelea na shughuli zako.Hilo
litaongeza upendo na amani kwenye nyumba.
Wanawake wengi wamejisahau sana na kuacha wanaume wafanye kila kitu
wenyewe jambo ambalo husababisha wanaume wengine watoke nyumbani bila
kupiga pasi au kusahau kuchana nywele.
Jirekebishe kama una tabia za kutojali usafi wa mwenza wako,
utanashati ni muhimu kwa wanaume pia usiishie kwa wanawake kujipenda
na kujiremba kila wakati huku wakisahau waume zao

No comments:

Post a Comment