Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam leo
na Kaimu Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano kutoka Wakala wa Vipimo
Tanzania (WMA), Irene John wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wajasiriamali
yaliyoandaliwa na Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) cha Wajasiriamali Wanawake
Tanzania (TASWE).
John alisema wajasiriamali wengi nchini
wamekuwa wakishindwa kuyafikia masoko ya kimataifa kutokana na vifungashio vyao
kukosa vipimo sahihi.
“Huwezi kufikia soko la kimataifa kama utatumia vipimo sahihi
kama kitu ni cha kilo moja weka kwenye ujazo wa kilo moja kwa kufanya hivi
utaweza kujitangaza na kuifanya biashara yako kuwa kwenye kiwango sahihi,” alisema
John na kuongeza kuwa matumizi ya ujazo usio sahihi sio tu yanawanyima
kujulikana katika soko la kimataifa, bali yanaweza kuwaumiza wajasiriamali au walaji.
“Kuna ambao wanatumia chupa za maji kufungasha bidhaa zao,
lakini hawajui kama maji ni mepesi na ujazo wake wake hauwezi kulingana na
asali hivyo unaweza kujinyima wewe kama mjasiriamali au ukamnyima mlaji,”
aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWE,
Anna Matinde alisema maonesho hayo yameshirikisha wajasiriamali 192 kutoka nchi
mbalimbali ikiwemo Comoro, Uganda, Rwanda, Kenya na wenyeji Tanzania.
Matinde alisema maonesho hayo ni muhimu
kwa kuwa yanasaidia nchi zilizoshiriki kubadilishana uzoefu katika utengenezaji
wa bidhaa mbalimbali.
Aidha, alisema ili kuhakikisha elimu ya
ujasirimali inafika katika nchi za Afrika Taswe inajenga chuo cha mafunzo
Comoro ili kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa bidhaa za Tanzania.
Naye Ofisa Ukuzaji wa Biashara kutoka
Mamlaka ya Uendelezaji Biashara Tanzania (Tantrade), Judith Matage alitoa mwito
kwa wajasiriamali hao kuyatumia maonesho hayo kujitangaza na sio kuuza bidhaa
pekee.
“Hii ni fursa lazima muitumie sio muuze tu sambazeni
mawasiliano kwa wajasiriamali kutoka nchi nyingine kwa kufanya hivi
kutawaongezea kujitangaza katika nchi mbalimbali,” alisema Matage.